3 Septemba 2024 - 15:36
WHO yasema watoto wa Gaza wanahitaji amani zaidi kuliko chanjo

Shirika la Afya Duniani la Umoja wa Mataifa (WHO) limesisitiza kuwa "amani" ndilo suluhisho bora zaidi la kuwaokoa watoto wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza, wakati kampeni ya chanjo ya polio ikiendelea katika eneo hilo ambalo linakabiliwa na vita vya mauaji ya kimbari vinavyotekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tedros Adhanom Ghebreyesus Mkurugenzi Mkuu wa WHO alisema katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumapili kwamba watoto huko Gaza wanapokea chanjo ya polio ndio, lakini hivi sasa chanjo inayohitajika zaidi ni watoto kupata amani.

Matamshi yake yamekuja wakati kampeni ya chanjo ikianza baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kukubali kusitisha kwa saa nane mashambulizi yake kwenye maeneo yaliyotengwa huko Gaza ili kuruhusu wafanyikazi wa afya kuwachanja mamia kwa maelfu ya watoto wa Kipalestina dhidi ya polio.

Kulingana na Rik Peeperkorn, mwakilishi wa WHO katika maeneo ya Palestina, kile kinachojulikana kama "usitishaji wa kibinadamu" kilianza Jumapili katikati mwa Gaza na hali hiyo itaendelea kwa siku tatu.Peeperkorn aliwaambia waandishi wa habari kupitia mkutano wa video siku ya Alhamisi kwamba kampeni hiyo inalenga kuwachanja watoto 640,000 walio chini ya miaka 10.

Tangazo la Alhamisi lilikuja baada ya mtoto wa miezi 10 kupooza baada ya kuambukizwa virusi vya polio.

Abdel-Rahman Abu El-Jedian, ambaye alizaliwa muda mfupi kabla ya vita vya Israel dhidi ya Gaza kuzuka Oktoba 7, alikuwa mmoja wa mamia ya maelfu ya watoto ambao walikosa chanjo kwa sababu ya vita.

Siku ya Jumatatu, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina lilisema watoto 87,000 wa Gaza wamepokea dozi ya kwanza ya chanjo ya polio huku zoezi la chanjo hiyo likiendelea kwa siku ya pili.

Utawala haramu wa Israel ulianzisha vita dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya harakati ya mapambano ya Kiislamu ya kupigania ukombozi wa Palestina, Hamas,  kuendesha mashambulizi ya kushtukiza ya Operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa dhidi ya utawala katili wa Israel ili kukabiliana na kampeni ya miongo kadhaa ya utawala huo ya umwagaji damu na uharibifu dhidi ya Wapalestina.

Vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Gaza hadi sasa vimesababisha vifo vya Wapalestina 40,786 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto na kujeruhi wengine 94,224. Maelfu zaidi pia wametoweka na inakisiwa kuwa wamekufa chini ya vifusi.



342/